BODI YA MIKOPO ELIMU YA JUU ZANZIBAR YASITISHA UTOAJI WA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kusimamisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, hadi hapo serikali itakapojiridhisha na utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo hiyo.

“Hatutatoa mikopo mwaka huu mpaka hapo tutakapokamilisha kazi ambayo tumeanza kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo ili kuhakikisha inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa wanaostahili,” alisema Dk Shein.

Akizungumza katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2015 na Kidato cha Sita mwaka 2016, Dk Shein alisema kuwa katika utaratibu wa sasa wapo waliodanganya kupata mikopo na ambao wamekopeshwa lakini wamekuwa wagumu kurejesha mikopo hiyo.

Katika hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na wengine 50 waliomaliza kidato cha sita, walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza katika mitihani yao ya taifa.

“Wako waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo mko 50 wa kidato cha tano mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la kwanza mtihani wa kidato cha nne,” alieleza Dk Shein na kuhoji msingi wa kukebehi matokeo hayo.


Aliongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi hao, ni sifa kwa Zanzibar na anaamini kwa hatua zinazochukuliwa na serikali kuimarisha miundombinu ya elimu pamoja rasilimali watu kiwango cha ufaulu kitazidi kuongezeka.

“Mnapofanya mitihani sote tunakuwa na wasiwasi, nyinyi wenyewe, walimu, wazazi na sisi serikali kwa kuwa tunaelewa kuwa matokeo yoyote yale ni yetu sote kama ni mazuri ni furaha yetu sote na kama si mazuri ni huzuni yetu sote,” Dk Shein aliwaambia wanafunzi hao.


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.