" MKOJO WA WEMA ULIKUA NA BANGI " - KESI YA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA.



Kesi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi inayomkabili mrembo Wema Sepetu jana aliendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo shahidi namba moja kwa upande wa mashtaka alitoa ushahidi wake na kusema kuwa mkojo wa mrembo huyo ulionyesha kuwa alivuta bangi.

Shahidi huyo, Elias Mulima kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akiongozwa na wakili wa serikali Constantine Kakula aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba namna alivyompima mtuhumiwa huyo na kubaini kuwa mkojo wake ulikuwa na bangi ambapo sampuli ya mkojo huo aliipokea Februari 8.

Shahidi alisema baada ya Wema kutoa sampuli ya mkojo huo ilipelekwa maabara ambapo lengo lilikuwa ni kuchunguza chembechembe za uwepo wa dawa za kulevya na ndipo walipobaini uwepo wa dawa za kulevya aina ya bangi. Baada ya kutoa ushahidi huo, Elias alitoa taarifa ya uchunguzi aliyoiandaa na kuisaini yeye mwenyewe na pia kuthibitishwa na kaimu mkemia mkuu wa serikali ili itumike kama kielelezo cha ushahidi.

Baada ya hoja hizo, upande wa utetezi unaoongozwa na Wakili Peter Kibatala aliitaka mahakama kutopokea taarifa hiyo kwa sababu uchunguzi haukufuata sheria kwani Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai inataka uchunguzi wa kitabibu kwa mtuhumiwa ambaye yupo chini ya ulinzi lazima upate kibali cha mahakama.

Aidha alitaka pia mahakama isipokee taarifa hiyo kwa sababu haikumbatanaishwa na fomu namba DCEA 001.

Akijibu hoja hizo, hakimu aliyekuwa mahakamani hapo alisema kuwa, fomu yenye namba 001 inatumiwa na Polisi wanaopeleka sampuli na fomu namba 009 ni taarifa ya mkemia, na kwamba fomu moja haitegemei nyingine kwa sababu huandaliwa na watu tofauti.

Hakimu pia aliipangua hoja ya Kibatala ya kibali cha mahakama ambapo alisema sheria haijasema kuwa wakati wote lazima Polisi waombe kibali hicho cha uchunguzi wa kitabibu, lakini pale ambapo mtuhumiwa atakuwa hayupo tayari, wanaweza kuomba kibali cha mahakama.

Kutokana na mvutano ulioibuka mahakamani hapo kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi, mahakama iliomba muda wa kupitia nyaraka hizo na kesi hiyo ikaahirishwa hadi Agosti 4 mwaka huu.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.