# EURO 2016 UFARANSA .. MAMBO MAKUU MANNE YAKUFAHAMU KUHUSU ENGLAND
ShaffiDauda
07 June 2016
Unapozungumzia mataifa makubwa katika soka ulimwenguni, basi hutoacha kuitaja England. Ni moja ya mataifa yanapambana kwa kiasi kikubwa kutafuta ‘glory’ kwa ajili ya watu wake lakini hata hivyo mara nyingi juhudi zao zimekuwa zikigonga ukuta.
Kwa kipindi kirefu sasa England wamekuwa hawafanyi vizuri sana kwenye michuano mbalimbali duniani ama Kombe la Dunia au Mashindano ya Ulaya (Euro).
Wamekuwa wakiishia katika hatua za awali na hatimaye kutupwa nje licha ya kikosi chao kusheheni mastaa mbalimbali wanaocheza katika ligi yao ambayo ni moja ya ligi bora ulimwenguni.
Kulelekea ufunguzi wa michuano ya Euro mwaka huu ambayo itapigwa nchini Ufaransa, nimekusogezea mambo manne muhimu ya kuyafahamu juu ya timu ya taifa ya England.
Miaka 50 ya Maumivu
Mwaka huu England wanatimiza miaka hamsini (50) kamili tangu kutwaa taji katika mashindano makubwa Ulaya na duniani. Ushindi wa kombe la Dunia katika ardhi ya nyumbani mwaka 1966. Wakati huo timu ikiwa chini ya meneja Alf Ramsey na nahodha wake Bobby Moore ikichagizwa na morali ya nyota wa United wakati huo Bobby Charlton.
Katika kundi lao England walikuwa na timu za Uruguay, Mexico na France. Waliitoa Argentina robo fainali, kabla ya kuwang’oa tena Ureno nusu fainali na kuwakatakata Ujuremani ya Magharibi wakati huo katika fainali iliyopigwa Wembley. England walishinda mabao 4-2.
Shukrani za pekee kwake mshambuliaji wa West Ham wakati huo Geoff Hurst ambaye alipiga hat-trick na kuwa mchezaji wa kwanza na wa mwisho mpaka sasa kufunga mabao matatu katika fainali ya kombe la dunia.
Licha ya kuonyesha kiwango cha juu katika miaka tofauti tofauti, England imekuwa ikiishia nusu fainali ama chini ya hapo kwenye michuano mbalimbali mikubwa…mwaka 1990 nusu fainali ya kombe la dunia, 1968 na 1996 nusu fainali ya Euro.
Tangu hapo wamekuwa na nyakati ngumu, ikumbukwe tu kwenye fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 walitupwa nje baada ya michezo miwili tu ya makundi.
Rooney anafukuzia kuvunja rekodi nyingine England baada ya ile ya Bobby Charlton
Nahodha wa timu hiyo Wayne Rooney alivunja rekodi ya Charlton ya kufunga mabao 50 kwa England Oktoba mwaka jana alipofunga goli la penati wakati wa mchezo wa kufuzu Euro dhidi ya Uswizi.
Rooney (31) ambaye kwa sasa ana magoli 52, anatarajia kuvunja rekodi ya kucheza michezo mingi kwa wachezaji wa ndani na kumzidi David Beckham ambaye alicheza mechi 115 endapo England itafika hatua ya mbali zaidi. Kwa sasa Rooney ameshaichezea England mara 111.
Kuwaamini vijana
Baada ya kuona wakongwe kama John Terry, Rio Ferdinand, Ashley Cole, Steven Gerrard na Frank Lampard wakistaafu kwa mpigo, Hodgson ameamua kuwekeza katika damu mpya na changa.
Kwa sasa ana vijana kadhaa ambao ni chachu ya ushindi wa timu hiyo, nyota watatu wa Tottenham ambao wamekuwa wakifanya vizuri Harry Kane (22) anaongoza jahazi katika safu ya ushambuliaji, Delle Ali (20) kwenye nafasi ya kiungo na Danny Rose (25).
Vijana wengine ni kama vile nyota wa Everton John Stones (21) na Ross Barkley (22), kiungo mkabaji wa Spurs Eric Dier (22) na Raheem Sterling (21) wa Manchester City.
Maumivu ya EURO mwaka 1996.
Mara ya mwisho England kufika katika hatua nzuri kwenye michuano hii ilikuwa ni mwaka 1996 ambapo walicheza katika ardhi yao ya nyumbani.
Kwenye makundi walizifunga Scotland 2-0 na Uholanzi 4-1, wakawang’oa Uhispania kwa matuta robo fainali kabla ya kugotea nusu fainali baada ya kufungwa na Ujerumani kwa namna ya kipekee.
Alan Shearer na Stefan Kuntz walianza kuifungia England mabao lakini hata hivyo baadaye Ujerumani walisawazisha, lakini almanusura wapate goli katika muda wa ziada lakini umakini mdogo wa Gascoigne uliinyima England ya kupata goli hilo.
Kwenye matuata ndipo England walipotoa machozi baada ya Gareth Southgate kukosa mkwaju uliookolewa na Andreas Kopke na kuwatupa nje ya mashindano England ambao walikuwa katika ardhi yao ya nyumbani.
No comments:
Post a Comment