MAJAMBAZI WATWANGANA RISASI WAKIDHANI NI POLISI, SILAHA ZA KIVITA ZA KAMATWA



Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wa kutumia silaha, ambao wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu katika mkoa wa Dar es Salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Licha ya kuuawa kwa majambazi hao, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwakamatwa watu zaidi ya saba, wanaosadikiwa kuhusika na tukio la majibizano ya risasi na polisi, lililotokeo Vikindu lililosababisha kifo cha askari mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.

Alisema watu hao walikamatwa kufuatia tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29, mwaka huu katika Jengo la Sophia House maeneo ya Veta Changombe, ambapo majambazi hao walidaiwa kupora Sh milioni 35 na kutoweka kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah lenye namba bandia T 549 BPK.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo, uliendelea kufanyika na Septemba 3, timu ya upelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, iliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata majambazi hao watatu na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa kutumia silaha na kuweza kutaja silaha mbalimbali walizonazo.

Kamanda Sirro alisema majambazi hao, waliwapeleka askari eneo la Mbezi Chini katika nyumba waliyokuwa wamekodi na askari walifanya upekuzi na walifanikiwa kupata silaha mbalimbali, zikiwemo bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu vinginevyo.



Alitaja silaha hizo kuwa ni bunduki za kijeshi tatu aina ya SMG zikiwa na magazini nane na risasi 120, bastola 16, magazini tatu za bastola na risasi moja, Shot gun pump action tatu na risasi 130, bastola 16 magazini na risasi 548 na bunduki tatu aina ya Shot gun na risasi zake 130.

Aidha alisema walikuta redio za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea mbali tatu, pingu za plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi mmoja wa kukatia vyuma, mtarimbo mmoja, risasi baridi za kutishia 37, boksi moja la kusafishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine moja ya kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.


Alisema uchunguzi wao ulibaini kuwa majambazi hao Septemba 6, mwaka huu walipora bunduki aina ya Shot gun yenye namba 006091830, ikiwa na risasi moja katika barabara ya Mbozi Chang’ombe.

Sambamaba na hayo, majambazi hao walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha katika Benki ya Habib African ya Kariakoo mwaka 2014 na Benki ya Stanbic mwaka 2014, wakitumia gari aina ya Toyota Noah.

Kamanda Sirro alisema baada ya mahojiano zaidi, majambazi hao walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.

Alisema askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo, walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele majira ya usiku.

Aliongeza kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.