Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amewataka vijana waliopo masomoni na wahitimu nchini, kuhakikisha wanajifunza zaidi mbinu za kujiajiri na si kusubiri kuajiriwa.
Aidha Waziri huyo, ametoa changamoto kwa taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu kuzalisha wahitimu wenye taaluma na mikakati itakayowezesha kujiajiri na si wahitimu wanaotafuta ajira.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Nicholaus Burreta wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Vijana, linalohusu mikakati ya kumaliza tatizo la ajira na rushwa.
“Ni kweli tatizo la rushwa ni kubwa si hapa nchini bali Afrika nzima kwa ujumla. Afrika ina watu takribani bilioni moja lakini kati yao milioni 50 hawana ajira. Nawapongeza vijana kwa kuliona hili na kuamua kulivalia njuga ili kulipatia ufumbuzi,” alisema.
Alisema wakati dawa ya ukosefu wa ajira ikiendelea kutafutwa duniani kote, ni wakati sasa kwa vijana wa kitanzania kuwa na mabadiliko ya kifikra na pindi wanapohitimu wajitahidi kuwa na elimu ya ziada itayowawezesha kujiajiri na si kusubiri ajira.
“Nasema tuachane na wasomi wanaosubiri ajira, hata taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu tutengeneze vijana wenye mitazamo chanya ya kujiajiri wenyewe. Hili si tu litawakwamua kiuchumi lakini pia litaongezea na kulijenga taifa kiuchumi,” alisema.
No comments:
Post a Comment