YANGA YAWASHTUKIA SIMBA


Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa 

Dar es Salaam. Vita ya ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara imekaa vibaya baada ya uongozi wa Yanga kudai umeshtukia njama za Simba za kutaka kuivuruga timu yao.

Wakati kukiwa na taarifa za chinichini za wachezaji wa Yanga wamepanga mpango wa kugomea mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Algier nchini Algeria ili kuushinikiza uongozi kuwalipa malimbikizo ya mishahara yao kwanza.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amekiri wachezaji kutolipwa mshahara wa Machi, lakini akasisitiza, klabu inajipanga ili kuwafanikishia malipo hayo wachezaji.

“Ni kweli wachezaji wanadai mishahara ya mwezi uliopita umechelewa. Pia kuna deni la nyuma na yote tumezungumza nao na watapewa siku si nyingi.”

“Yanga siyo klabu ya kwanza au kampuni ya kwanza kuchelewesha mishahara, nadhani hata wewe mwandishi kwenye kampuni yako mambo hayo yametokea na huenda yanatokea. Hivyo ni mambo ya mpito,” alisema Mkwasa.

Alifafanua kwamba kuhusu kugoma kwa wachezaji wao hakuna ukweli na kudai kupata taarifa za uvumi huo kuchochewa na watu wa Simba ambao hakuwataja majina.

“Taarifa tunazo kwamba uvumi unaoendelea dhidi yetu unachochewa na watu wa Simba, ili mradi watuvuruge na wanachama wetu, lakini nasisitiza tena Yanga ipo imara.

“Wachezaji wetu wote watakwenda Algeria katika mchezo wa marudiano na ikitokea ambaye hatakwenda, basi si kwa sababu ya uvumi wa mgomo bali kutakuwa na jambo jingine hasa suala la majeruhi,” alisisitiza Mkwasa.

Kiongozi huyo aliyewahi kuwa mchezaji, kocha na sasa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, alikiri mtikisiko wa uchumi kuchangia kuchelewa kwa mishahara ya wachezaji wao, lakini akasisitiza kwa mara nyingine kwamba siku si nyingi kila kitu kitakuwa sawa.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.