VILIO VYA FURAHA VYASIKIKA BAADA YA MADEREVA WALIOTEKWA DRC KUWASILI NCHINI +PICHA



Vilio vya furaha kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki, vimetawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana, baada ya kuwasili kwa madereva 10 wa Tanzania waliotekwa na kunusurika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Madereva hao waliwasili katika uwanja huo saa 9 alasiri, wakitoka Kigali, Rwanda kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda na kukutana na familia zao kwa mara ya kwanza baada ya kuokolewa.

Wakiwa uwanja wa ndege, walizungumza na waandishi wa habari na kueleza namna walivyotekwa na waasi waliovalia sare za jeshi zisizofanana na walivyosafirishwa zaidi ya kilometa 50 porini usiku na mchana, wakitembea kwa magoti na kupoteza tumaini la kupona huku baadhi wakifanikiwa kutoroka na wengine kuokolewa.

Kabla ya kuwasili kwa madereva hao, ndugu zao walikusanyika uwanjani hapo wakiwa na shauku ya kukutana na madereva hao ambao Septemba 14, mwaka huu, walikumbwa na kadhia ya kutekwa na kundi la wanamgambo huku magari waliyokuwa nayo yakichomwa moto na hatma yao kutojulikana.

Hata hivyo, kutokana na juhudi za Serikali ya DRC na Tanzania, madereva hao walifanikiwa kuokolewa na kupatiwa matibabu ambapo jana walirejea nchini rasmi.


Baada ya madereva hao kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari, walitoka nje kwenda kuonana na ndugu zao waliokuwa wamekusanywa pembeni, lakini walipowaona tu walishindwa kujizuia na kuwakimbilia madereva hao ambao nao waliwakimbilia huku wakilia na kutamka maneno ya kumshukuru Mungu kwa kuonana tena.


Baadhi ya familia ziliambatana na watoto wa madereva hao, ambao katika hali ya kutia simanzi baada ya kuwaona wazazi wao, waliangua kilio kwa sauti huku wakiwaita baba zao na kuwakumbatia kwa furaha.


Madereva waliookolewa kutoka Tanzania na waliowasili jana ni Kumbuka Selemani, Hussein Mohammed, Bakari Nassoro, Issa Omary, Amdani Zarafi, Adam James, Mbwana Said, Ali Juma, Athuman Fadhil na Amis Mshana.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.