FRIDAY XO : KUMCHUKIA EX WAKO NI KUPOTEZA MUDA WAKO



Mapenzi yana siri kubwa. Kila mmoja ana ugonjwa wake wa kupenda. Wengine wanawapenda wapenzi warefu, lakini kuna kundi ambalo huchanganyikiwa zaidi kwa wafupi. Pamoja na mchanganuo huo, kuachwa inauma hata kama anayekutosa hukuwa na mapenzi naye.

Ile dhana tu ya kuachwa ndiyo hutesa watu. Kuna dhana kwamba anayeacha mara nyingi hujiona mshindi dhidi ya aliyemuacha. Na hiyo ndiyo sababu ya wengi kuumia wanapofungiwa milango ya kukatisha uhusiano ambao pengine hata hawakuwa na maslahi nao. 

Watu wanaingia kwenye mapenzi na baadaye wanatengana. Wapo wanaobaki na amani, lakini wengine wanaendelea kuishi katikati ya chuki.

Husalimiani na mwenzi wako wa zamani, mbaya zaidi pengine huyo uliye na uhasama (bifu) naye, mmefanikiwa kupata mtoto pamoja. Usiangalie moyo wako, zingatia ukuaji wa mwanao.



Hapa nifafanue kitu kimoja kwamba sifundishi watu kuwakaribia wenzi wao wa zamani, la hasha! Nashauri kutowekeana uadui kwa sababu hauna maana.

Mtaalamu mmoja wa saikolojia ameandika: “Moja kati ya njia rahisi ya kupoteza muda wako ni kumchukia mwenzi wako wa zamani.” 

Binafsi nakubali, kwa nini ujenge bifu na mtu aliye nje ya mzunguko wako wa maisha? Naweza kuelewa kwamba kumchukia mtu ambaye hayupo tena kwenye mzunguko wa maisha yako, ni kama hatua ya kujipa maumivu ya moyo au huzuni isiyo na sababu.

Ukimchukia mwenzi wako wa zamani, maana yake unaendelea kumhifadhi kwenye moyo wako. Aghalabu utakumbuka mabaya yake lakini kuna vipindi vichache ambavyo mazuri yake yatakujia.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.