MAONI YA WANAFUNZI, WAHADHIRI NA WAZAZI - TCU KUSITISHA VYUO 19 KUDAHILI WANAFUNZI WAPYA


Image result for tanzania commission for university

Baadhi ya wamiliki wa vyuo vikuu nchini, wanataaluma, wanafunzi na wazazi wametikiswa na taarifa ya Serikali ya kuzuia kufanyika kwa udahili wa vyuo na baadhi ya kozi za masomo kwa muhula ujao kutokana na kasoro mbalimbali.

Jana, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilitoa taarifa kwa umma inayoeleza hatua iliyochukua ya kusitisha udahili wa wanafunzi wapya katika vyuo 19 na pia kozi za masomo 75 zilizokuwa zikitolewa kwenye vyuo mbalimbali nchini.

Taarifa hiyo ya TCU, ambayo ilitolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wake, Prof. Eleuther Mwageni, ilifichua sababu ya kuchukua uamuzi huo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa sifa katika vyuo husika.

Miongoni mwa vyuo vilivyoguswa kwa namna mbalimbali na uamuzi huo wa TCU ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dodoma (UDOM), KCMC, Tumaini, Ruaha, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), Kampala kampasi ya Dar es Salaam (KIU) na IMTU.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wanafunzi ambao kozi wanazosomea zimefutiwa udahili walisema wameshtushwa na hatua hiyo na kuwapa hofu kuwa pengine, hata kama wao hawajaguswa moja kwa moja, hali hiyo inawapa hofu kuwa pengine sifa zao zitakuja kutiliwa shaka.

“Inashtusha kwa sababu kama kozi unayosomea umeambiwa kuwa haina sifa kutolewa na chuo chako, maana yake hata wewe unakuwa hujiamini tena. Unaweza kujawa hofu kuwa hapo baadaye itakuja kauli nyingine inayoweza kufuta sifa hata za kile mnachoendelea kukisomea,” mmoja wa wanafunzi aliiambia Nipashe.

Aidha, baadhi ya walimu wa kozi za masomo yaliyofutwa kwa kukosa sifa kwenye vyuo vyao waliiambia Nipashe kuwa tangazo hilo la TCU limewaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu wanajua kuwa kwa waliopo, ajira zao zitakuwa shakani.

“Wanafunzi wapya wasipodahiliwa, maana yake chuo kitalazimika kupunguza baadhi ya watumishi wakiwamo wahadhiri wasaidizi na hilo linatishia mno ajira zetu,” alisema mmoja wa wahadhiri wasaidizi, lakini akikataa kuilaumu TCU kwa hatua waliyochukua.

Maoni tofauti kuhusiana na tangazo hilo la TCU yalitolewa pia na baadhi ya wazazi na wamiliki wa vyuo, wengine wakiunga mkono kwa kuwaepushia hasara endapo wangedahili watoto wao katika vyuo au kozi kwenye vyuo visivyo na sifa huku wengine wakilaumu kwa kutaka serikali kuvipa muda wa kutosha vyuo husika ili kushughulikia kasoro zilizoainishwa na hivyo kutoa fursa ya kudahiliwa kwa wanafunzi wapya.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARco), Danford Kitwana, alisema vyuo hivyo vitaathirika kifedha kwa kuwa vilishaweka bajeti na vinajiendesha kwa kutegemea ada za wanafunzi.

Alisema vyuo vidogo vitaathirika zaidi kwakuwa idadi ya wanafunzi itapungua na kushindwa kujiendeshwa kwa programu chache zilizobaki.

“Ilitakiwa kabla wangetangaza ili kila mmoja ajue anawekeza vipi,” alisema.

Alisema baadhi ya vyuo vimeshatumia mamilioni ya fedha kwa kutangaza progarmu hizo kwa lengo la kupata wanafunzi
“Kama TCU wamefanya kwa kuzingatia vigezo halisi, itakuwa sawa.


Lakini kwa TUDARCo kuna malalamiko. Wamesitisha shahada ya uzamili kwa madai kuwa inafundishwa na walimu wa Shahada ya Uzamili wakati ukweli inafundishwa na wakufunzi wenye shahada za Uzamivu wakiwa wa kudumu na wengine wa muda mfupi,” alisema.

Alisema athari nyingine ni kwa wanafunzi ambao watakosa nafasi za masomo na hivyo kusubiri hadi mwakani, na kwamba vilivyopo havitoshelezi kwa kuwa vina idadi maalumu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alisema kilichofanywa na TCU ni utekelezaji wa sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005, inayotaka kufanyika uhakiki katika maeneo ya taaluma ili kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.

“Sekta ya elimu ya juu imekua sana. Kuna vyuo vingi nchini hivyo uhakiki umefanywa na kuthibitisha kuna vyuo havikidhi haja… ili kuimarisha sekta ya elimu ya juu, kuboresha kiwango cha elimu, ni lazima kuimarisha taasisi ziwe na uwezo wa kuendesha hizo programu,” alisema.

Alisema baadhi ya vyuo vilibainika kuwa na uwezo mdogo wa kutoa elimu katika maeneo mengine hivyo kwa sasa wanaweza kutoa kwa ngazi za chini ambazo hazikuwa na uwekezaji wa kutosha.


Source : Nipashe. 

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.