MAGUFULI KUKISUKA UPYA CHAMA CHA MAPINDUZI.. ATISHA VIKAO VYA CC NA NEC DECEMBER 13



Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), inatarajia kukutana Desemba 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam, imefahamika.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Msemaji wa chama hicho, Seleman Mwenda, ilisema mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Desemba 11 hadi 12, jijini Dar es Salaam.

Ingawa hadi sasa ajenda za vikao hivyo hazijajulikana, lakini wachambuzi wa masuala ya  siasa wanasema, kufanyika kwa vikao hivyo kunatajwa kuwa ni mkakati wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli  kutaka kuisuka upya CCM.

Baadhi ya wachambuzi hao wanasema uteuzi wa wajumbe watatu wa sekretarieti ya chama hicho kuwa mabalozi ni mwendelezo wa mkakati huo kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho mwakani.

Mbali na hao mjumbe mwingine wa sekretarieti, Dk Asha -Rose Migiro aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na nafasi yake ndani ya chama kuchukuliwa na Pindi Chana ambaye naye ameteuliwa kuwa balozi.

Katika hotuba ya Rais Dk. Magufuli baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho alisema miongoni mwa mambo atakayoyatekeleza ni kuimarisha utendaji kazi wa chama, huku akimnukuu hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kusema kuwa chama legelege huzaa serikali legelege.

“Nitashirikiana nanyi kujenga chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya katiba na kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo.

“Tutahakikisha pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia shina hadi taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi” alisema Dk. Magufuli.


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.