Benki ya Dunia Yaunga Mkono Sera ya Elimu Bure kwa Kutoa Bilioni 181 .
BENKI ya Dunia (WB) imekubali kusaidia utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo kwa Serikali ambapo imetoa dola milioni 80 sawa na Sh bilioni 181.
WB imefikia uamuzi huo baada ya kuona mwitikio mkubwa wa wanafunzi kujiunga na shule za msingi, hali inayoonesha kuanza kuilemea Serikali kutoa elimu hiyo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.
Mkurugenzi Mkaazi wa WB kwa Tanzania, Somalia, Malawi na Burundi, Bella Bird alibainisha jana kwamba fedha hizo zimetolewa na taasisi ya International Development Association (IDA) inayokwenda na mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Lengo ni kusaidia Serikali kukabiliana na changamoto inazokutana nazo katika mpango huo wa kutoa elimu bila malipo,” alisema.
Alisema pia lengo la lingine la kutoa fedha hizo ni kusaidia kuhudumia ongezeko la watoto wanaoijunga na shule pamoja na elimu bora itakayosaidia Taifa baadaye.
“Mpango wa elimu bila malipo ni jambo la kusaidia Serikali kufikia malengo ya kuwapa watoto wa kitanzania elimu, hivyo sisi WB tumeamua kuongeza nguvu ili Serikali isikwame,” alisema.
Bird aliipongeza Serikali kuondoa vikwazo katika utoaji elimu, hivyo kusababisha makundi yote kupata elimu bila tatizo lolote.
Mkurugenzi huyo alisema ni dhahiri uamuzi huo utasababisha ubora wa elimu huku dhana ya utekelezaji lengo la elimu kwa wote ikikamilika, kwa kuwa hakuna atakayeachwa nyuma.
“Tunaamini kuwa kupitia msaada huu, ni matumaini yetu kuwa Mamlaka itahakikisha kuwa watoto wanapata elimu hasa ambao wanaishi katika mazingira magumu,” alisema.
Alisema mpango huu ulianza mwaka 2014 ambapo WB ilipitisha dola milioni 122 ili kuhakikisha kuna elimu bora kwa shule za msingi na sekondari.
Msaada huo wa WB ni mwendelezo wa benki hiyo kutoa misaada kwa nchi ambapo hivi karibuni Rais wake, Dk Jim Yong Kim alizuru nchini na kuweka jiwe la msingi la daraja la juu Ubungo, Dar es Salaam ambao utagharimu zaidi ya Sh bilioni 188.71 msaada kutoka benki hiyo.
Aidha, WB hadi sasa inafadhili miradi zaidi ya 28 nchini ukiwamo ujenzi wa barabara ya mwendo kasi kwa gharama ya zaidi ya dola bilioni 4.2 ambapo Tanzania itarudisha kwa riba ndogo ya asilimia 0.5
No comments:
Post a Comment