KAMPUNI ZA SIMU ZISIZOJISAJILI DSE KUFUTIWA USAJILI
Rais John Magufuli ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuta kampuni za simu za mkononi zote ambazo hazitaki kujiandikisha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Aidha, amezitaka kampuni mbalimbali kujisajili katika mfumo wa ukusanyaji kodi za serikali kwa njia ya kielektroniki, aliouzindua jijini Dar es Salaam jana, mfumo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Tulipitisha sheria kwamba makampuni ya simu yote lazima yasajiliwe kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, wamesuasua weee, wamezunguka …TCRA msitoze faini, futeni hizo kampuni,”alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa faini ambayo imewekwa na TCRA ni ndogo, hivyo kampuni hizo haziogopi.
Alisema kituo hicho kilichoanza kazi Oktoba mwaka jana, mwitikio wa kujiunga sio mkubwa, ambapo ni kampuni tatu pekee ambazo zimejiunga na alihimiza zingine kujiunga.
Rais Magufuli alisema kwa kutumia kituo hicho, makusanyo ya kodi hayatakuwa na malalamiko tofauti na huko awali kulikuwa na malalamiko kwa wakusanya kodi na pia walipa kodi wakidai kuongezewa viwango.
“Tulikuwa tukitumia makusanyo ya kodi ya mtu na mtu na huyo mtu inategemea uaminifu wake, wapo ambao sio waaminifu wanapokwenda kwa wateja wanawakadiria makadirio ya juu na pia walipakodi kudanganya wanachopata,”alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema mwarobaini wa malalamiko hayo ni mfumo huo, ambao ni mashine zinakokotoa na kwamba hakuna mwingilio wa mtu katika hesabu.
“Wengine wote ambao hamjajiunga mfanye hivyo kwa hiari, mlipa kodi na mkusanya kodi mnatakiwa kuishi kwa raha na upendo,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa kama wafanyabiashara hao wanataka mpaka sheria ibadilishwe ndipo watii agizo hilo, serikali inaweza kupeleka muswada kwa hati ya dharura.
“Najua mnaweza kufafuta visababu kama mnataka mpaka tubadilishe sheria bado Bunge linaendelea kule, tunaweza kufanya mabadiliko,” alisema na kuziomba kampuni hizo kushirikiana na serikali, isionekane kwamba serikali haitaki kushirikiana na wawekezaji kwa kuanzisha mfumo huu.
Aidha, alisema serikali hii inawapenda wawekezaji ndio maana inawawekea mazingira bora ya biashara sambamba na ukusanyaji kodi ulio sahihi.
“Niwaombe ndugu zangu, na hii nawaomba kutoka moyoni mwangu tunahitaji kodi, nchi zote zinalipa kodi, ni lazima kila mmoja alipe kodi awe anataka au hataki,” alisema.
Rais Magufuli aliziomba kampuni za simu pamoja na kampuni nyingine, kuingia katika mfumo huo ili kuwe na usawa katika ukusanyaji wa kodi.
Alisema anachukia wawekezaji pamoja na ubinafsishaji wa mali za umma wa hovyo, ambao hauna faida kwa nchi ambapo alisema kuna zaidi ya kampuni 197 zimekufa.
“Naeleza yote haya ili muelewe serikali ninayoiongoza inataka nini, inataka kufanya biashara na wawekezaji ambao ni waaminifu, biashara yoyote lazima iwanufaishe na wenye nchi,” alisema.
Aidha, Rais Magufuli alizitaka wizara zote zisimamie kampuni kuingia katika mfumo huo, ambao utawasaidia pia katika biashara zao kujua mapato yao.
“Hakuna mtu duniani anayependa kulipa kodi, hata enzi za Yesu, na walipa kodi katika enzi zote hawakupendwa, usitegemee wewe kamishna TRA, ZRA utapendwa, wewe kusanya tu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema nchi inapoteza fedha nyingi kupitia mianya ya upotevu wa mapato, lakini serikali iliamua kujenga kituo hicho kwa lengo la kuhakikisha na kulinda usalama wa taifa na taasisi za serikali na kampuni binafsi pamoja na kuimarisha na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Kampuni ambazo zitatunza taarifa zao kwenye kituo hiki zitakuwa na uhakika wa usalama wa taarifa zao hata kama uharibifu wowote utatokea,” alisema.
No comments:
Post a Comment