RC GAMBO, WADAU WA UTALII WAWEKA MKAKATI KUIPAISHA ARUSHA
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo amekutana na wadau wa sekta ya utalii mkoani humo na kujadili nao namna mbalimbali wanazoweza kuboresha sekta ya utalii mkoani humo.
"Mkoa wa Arusha unachangia mapato ya utalii nchini kwa zaidi ya asilimia 80 hivyo sisi kama mkoa tukiwa na mikakati madhubuti ya kuiboresha hii sekta tutakua tumeikuza sekta hii kiasi cha kuleta matokeo chanya kwa taifa kiujumla." Alisema Gambo.
Nao chama cha wafanyabiashara wa utalii (TATO) walisema changamoto katika biashara hiyo ni nyingi lakini kwa sehemu kubwa wanaishukuru serikali ya awamu ya tano kwani katika awamu hii changamoto nyingi zimeonekana kutatuliwa, kwa kuongezea walisema kinachowapa hofu kwa kipindi hii kuelekea mwaka mpya wa fedha ni kuanza kwa tozo mpya ya ada ya mahoteli yanayolaza wageni porini (concession fee) ambapo wao kama walaji wa mwisho wanaona itawaathiri sana kwakua tangazo la serikali limetoka ndani ya muda mfupi, "tangazo limetoka mwezi mei na wageni walishafanya booking toka mwezi machi na tuliwapa bei zisizokua na tozo hizi, hivyo tunaomba serikali ilifikirie hili mara mbili na kutuongezea muda tuanze kulipa januari ili isituathiri kibiashara." Alisema bwana Willy Chambulo mwenyekiti wa TATO.
Akiwatoa hofu hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA bwana Allan Kijazi amekiri kua hiyo tozo kwa wakati ni changamoto ila akawatia moyo kuwa bado kuna muda wa kulizungumza hilo kwani serikali hii ya awamu ya tano ni sikivu, na aliwataka wakutane wadau wote wajadiline waone namna ya kuishauri wizara kuongeza muda ili isiathiri biashara hii kwa ujumla.
Naye Mhe Gambo amewachagiza wadau hao kushirikiana na viongozi wa mkoa kuandaa tamasha kubwa la utalii la kimataifa litakalotumika kama jukwaa la kuutangaza mkoa na taifa kwa ujumla hasa kwa kualika mabalozi wa nchi ambazo huleta watalii wengi hapa nchini, vilevile akatoa rai kwa wageni wawe na amani wawapo mkoani hapa kwani kwa sasa mkoa ni shwari na kamati yake ya ulinzi na usalama imejikita katika kuzima viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.
Vile vile Mhe Gambo amepokea jumla ya mablanketi 200 kati ya 400 kutoka Leopard tours na kuyabidhi kwa jeshi la magereza kwaajili ya wafungwa katika gereza kuu Kisongo,pia amekabidhi kompyuta moja na printer kwa wafungwa wa gereza hilo la Kisongo ikiwa ni katika utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wafungwa hao kipindi alipowatembelea mapema mwezi wa tano.
No comments:
Post a Comment