ATLETICO MADRID INAVYOKOSESHWA RAHA NA MANAHODHA WASAIDIZI (JEZI 04), HISTORIA IMEELEZA

MANAHODHA WASAIDIZI(JEZI NAMBA 4) MKOSI KWA ATLETICO MADRID UEFA- HISTORIA IMEELEZA HIVYO.
Ratiba ya mechi za nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya imetoka na kushuhudia mabingwa mara kumi, Real Madrid, ambao wamecheza nusu fainali nyingi zaidi (26, kushinda 13 na kushindwa 13) wakipangwa na ingizo jipya kabisa kwenye hatua hii, Man City, huku mabingwa mara tano, Bayern Munich, ambao wameshacheza nusu fainali 17 (kushinda 10 na kushindwa 7) wakipangwa kukutana na wanafainali mara mbili, Atletico Madrid, ambao wameshacheza nusu fainali 4 (kushinda 2 na kushindwa 2).
Ukiiacha City ambayo kufika kwao nusu fainali ni mafanikio makubwa zaidi, ni Atletico pekee ndiyo wenye kulihitaji zaidi kombe hili kuliko wana nusu fainali wengine. Hii inatokana na ukweli kwamba Atletico wameteseka sana kulitafuta kombe hili na kukutana na maumivu yenye kutia simanzi.
Wameshacheza fainali mbili na kupoteza zote katika wakati ambao wao wenyewe na hata dunia nzima ilishaamini kwamba Atletico ni mabingwa, kasoro mtu mmoja tu…beki mmoja wa kati wa timu pinzani ambaye ni nahodha msaidizi.
Miaka 42 iliyopita(1974), Atletico Madrid walikutana na Bayern kwenye fainali ya klabu bingwa Ulaya (kabla haijabadilishwa na kuwa ligi ya mabingwa Ulaya 1992).
Fainali hiyo iliyofanyika uwanja wa Heysel mjini Brussels Ubelgiji, ilishuhudia dakika 90 zikimalizika kwa suluhu na Atletico kupata bao la kuongoza ndani ya dakika 30 za ziada. mpaka dakika ya 120, sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho, Atletico walikuwa wakiongoza na walishaamini kwamba wameshinda hadi pale beki wa kati wa Bayern, Hans- Georg schwarzenbeck aliyekuwa akivaa jezi namba nne ambaye alikuwa nahodha msaidizi, alipofanya muujiza wa kutoka na mpira nyuma na kuachia shuti kali la mita 30 na mpira kujaa wavuni.
Wakati huo sheria ya mikwaju ya penati kuamua bingwa ilikuwa haijaanza kutumika hivyo mechi ilitakiwa irudiwe siku mbili baadaye. Atletico walikata tamaa na kujikuta wakipigwa 4-0 kwenye mchezo wa marudio.
Kwa kumbukumbu tu, Bayern hiyo ilikuwa inaundwa na nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani kama Schwarzenbeck mwenyewe, kipa aliyeogopewa Sepp Maier, binadamu wa pili na wa mwisho kuwahi kushinda kombe la dunia kama mchezaji na baadaye kocha, der Kaiser Franz Beckenbauer (wa kwanza ni Mario Zagallo wa Brazil), mlipua mabomu wa taifa Gerd Muller, Uli Hoenes na wengine wengi ambao mwaka huohuo waliiongoza Ujerumani kutwaa kombe la dunia kwa kuifunga Uholanzi ya Johan Cruyff na staili yao ya ‘Total Football’.
Miaka 40 baadaye yaani mwaka 2014, Atletico walitinga tena fainali na kukutana na majirani zao wa mji mmoja, Real Madrid.
Mchezo huo nao ulishuhudia Atletico wakiongoza mpaka dakika ya 4 ya muda wa nyongeza yaani 90+4 hadi pale beki mwingine wa kati (kama ilivyokuwa 1974) Sergio Ramos anayevaa
jezi namba nne ambaye pia alikuwa nahodha msaidizi wa Real Madrid alipoibuka kutoka kusikojulikana na kuisawazishia timu yake.
Bao hilo lilikuja katika wakati ambao wachezaji wa Atletico walikuwa wameshaamini kwamba wametwaa ubingwa kwa hiyo kuingia kwake kulivunja nyoyo zao na kujikuta wakipoteza kwa mabao 4-1 kwenye muda wa ziada.
Mwaka huu katika timu zilizoingia nusu fainali, hakuna timu yenye beki wake wa kati ambaye ni nahodha msaidizi…je Atletico wakifanikiwa kuingia fainali watapoza machungu yao?
Tukutane San Siro Milan May 28 lakini kwanza April 27 na May 3.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.