MAMBO MAKUU MATANO ( 5 ) YA KUIAMBIA NAFSI YAKO

Silhouette of businessman looking down


 Kujitambua katika maisha ni pale mtu anapokuwa  na uelewa binafsi wa kujing’amua yeye ni nani, anapaswa kufanya nini, kwa sababu ipi, lini na katika muktadha upi? Elimu hii ya kujitambua ni adimu mno! Kwani hujikita ndani ya nafsi ya mtu na kumfanya kuonekana mwenye busara na hekima katika uongeaji, kimaamuzi na kimatendo.

 1.Sina muda wa kutulia

Katika hali ya kawaida unaweza ukawa ulikutana na mambo yaliyokufanya uache kuwa mchakarikaji, mbishi na usiyekubali kushindwa katika kupigania mafanikio.

Nakuambia anza sasa kuamsha upya hisia za kupambana na vikwazo vyote vinavyokuzuia wewe kutimiza malengo yako na ukizingatia muda haukusubiri wewe.

 2. Nina kila sababu ya kuiamini nafsi yangu

Umeishi muda mrefu kwa kusikiliza sauti za watu wakikuambia wewe unapaswa uweje kulingana na mitazamo yao.

 Unapaswa ujue kuwa unapotaka kufanya jambo lolote mtu wa kwanza kumsikiliza ni nafsi yako ambayo siku zote haina muda wa kukudanganya. Si kwamba usisikilize ushauri kutoka kwa watu wengine, la hasha, ila unapaswa utangulize nafsi yako kwanza.

 3.Upekee wangu ndio nguvu yangu kuu

Ndio hujakosea, upekee wako ndio utakaokutofautisha wewe na mtu mwengine.

Yawezekana mazingira yalikuwa yanakufanya utake kuwa na tabia kama za fulani na hivyo ukajikuta unapoteza uhalisia wako. Anza sasa kuishi wewe na sio mtu mwengine.

 4.Nitatumia changamoto zangu kujiimarisha na sio kuniangusha

Hakuna mafanikio yasiyo na changamoto na ukiona changamoto inakuwa kubwa, basi ukishinda na mafanikio yake yanakuwa makubwa.

Yawezekana watu walikutendea uovu lakini wewe ukashikilia upendo dhidi yao. Badala ya kufunga mlango kuzuia changamoto katika maisha yako fungua ili ukutane nazo zikuimarishe.

5.Bado nina nafasi ya kujifunza zaidi hata kama nimeshindwa baadhi

Kitu kizuri kwako ni kuwa na moyo wa kutoruhusu anguko la mambo yaliyopita yaendelee kuzuia inuko la mambo yajayo.

 Dunia ina fursa nyingi za kujifunza moja, mbili au tatu zinaposhindikana inuka angalia nyingine zaidi na zaidi.

 Hakuna jambo kubwa linaweza kukamilika kwa siku chache, unapaswa uangalie njia mbadala bila kuchoka.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.