MAMBO MUHIMU KUFANYA WAKATI WA MWEZI WA RAMADHANI...


Siku za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zinazidi kusonga mbele ambapo unaendelea kumkumbusha ndugu muislamu kuendelea kufanya yafuatayo kwa nguvu zote.

Kusoma Qurani

 Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala); “Mwezi wa Ramadhani ambayo imeteremshwa ndani yake Qur-an hali ya kuwa ni uongofu kwa watu “ Kwa kuwa katika mwezi huu ndio Qurani iliteremshwa kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), inatakiwa kwa muislam kufanya bidii kuisoma angalau juzuu moja kwa siku ili aweze kumaliza msahafu ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Ramadhan.

 Kuharakisha kufungua

Miongoni mwa sunna tukufu zinazotakiwa kwa mfungaji katika mwezi huu kuzikimbilia, ni kuharakisha kufungua baada tu ya kuzama jua, kwani Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema katika hadithi iliopokewa na Tirmidhy, Ibnu khuzayma na Ibnu Habban, amesema Bwana Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam); “Hakika nimpendaye zaidi miongoni mwa waja wangu ni anayefanya haraka katika wao kufungua saumu.”

 Kuswali usiku

Inatakiwa kwa muislam kuyatumia masiku ya mwezi huu mtukufu katika kumuabudu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kusali na kufanya ibada nyengine, kwani ni mwezi wa pekee ambao ndani yake kunapatikana usiku wa cheo (Laylatul Qadr) ambao ibada ya usiku huo inalingana na ibada ya miezi elfu moja, na kwa hekima yake Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hakutubainishia kuwa ni usiku wa tarehe ngapi. Na hii ni moja miongoni mwa fadhila za kusali katika masiku ya mwezi huu. Vile vile mwenye kusimama kwa ibada katika masiku haya husamehewa makosa yake yote yaliotangulia,kama alivyosema Bwana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam): “Mwenye kusimama usiku wa Ramadhani kwa kufanya ibada hali ya kuwa na imani na kutaraji thawabu anasamehewa yoteyaliotangulia miongoni mwa makosa yake.” ( Bukhari na Muslim).

 Kula daku

Kula daku vile vile ni miongoni mwa sunna tukufu zinazodharauliwa na wengi kati ya waislam na fadhila zake ni kubwa kupita kiasi, miongoni mwazo ni kurehemewa na Allah na kutakiwa msamaha na malaika watukufu kama alivyosema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika hadithi; “Hakika Allah na Malaika wake wanawarehemu wenye kula daku.” (Twabrani, Ibnu Habban). Vile vile Bwana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesisitiza katika  hadithi  kwa kusema kuwa “Hakika daku ni baraka amekupeni Allah, hivyo basi musiiache”. (Annasai)

 Kukaa Itikaaf

Inatakiwa kwa muislam kuujaalia mwezi huu na kuutumia katika kuchuma na kuvuna aina tofauti ya mema ikiwemo Itikaaf, kwani ni miongoni mwa ibada bora sana zinazomkurubisha mja kwa  Mola wake (Subhaanahu wa Ta’ala) hasa awapo katika mwezi huu wa Ramadhani, kwani baadhi ya wanavyuoni wamesema kuwa haisihi ibada hii ya itikaaf pasi na funga. Na yatoshe malipo makubwa yaliotajwa katika hadithi; Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;“Mwenye kukaa itikaaf siku kumi katika mwezi wa Ramadhani, basi ni kama aliyehiji na akafanya umra mara mbili mbili.” (Bayhaq)

   Kutoa sadaka

Miongoni mwa ibada tukufu alizokuwa akizifanya Bwana Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni kutoa sadaka na alilipa umuhimu sana jambo hili hadi wakati wa kuondoka kwake ulimwenguni alipokuwa katika sakaratul mauti kila alipopata fahamu ilikuwa akimuuliza Bibi Aisha (‘Alayhis Salaam) iwapo ashazitoa sadaka  zile dirhamu nne zilizokuwa nyumbani? Kadhalika kutoa huku kwake kulikuwa kukiongezeka katika Ramadhani.

Kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)

Katika mwezi huu  wa Ramadhani kadhalika inatakiwa kwa muislam kuwa mengi ya maneno yake yawe katika kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani ni jambo ambalo linasaidia katika kuusafisha moyo wake na kuiboresha funga yake. Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ametuamrisha tumtaje kwa wingi katika aya nyingi za Qurani, na hii ndio ibada pekee aliyosema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa ifanywe kwa wingi, na miongoni mwa aya hizo; “Enyi Mlioamini mtajeni Allah kwa wingi na mumtakase yeye asubuhi na jioni.” (Al- Ahzaab 41 na 42)

Kadhalika Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alifundisha aina tofauti za kumtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ili tusichoke na jambo hili kwani mwanadamu ni mwepesi wa kuchoka na jambo moja tu. Vile vile akatuonyesha tofauti kubwa iliopo kati ya anayemtaja Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na asiyefanya hivyo kati hadithi aliposema; “Mfano wa anayemtaja Allah na asiyemtaja ni mfano wa mtu aliyehai na aliyekufa.”(Bukhari).

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.