CHADEMA: SIASA NI WAJIBU WETU... MANENO YA JPM HAYATUZUII KUFANYA WAJIBU

Freeman-Mbowe

Siku moja baada ya kuonywa na Msajili wa vyama vya siasa hapa nchini, Jaji Francis Mutungi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka na kusema, oparesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) ipo palepale

Jaji Mutungi, katika taarifa yake kwa siku ya jana alisema, “Tamko la Chadema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, linaloudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.” Alikuwa akizungumzia tamko la maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe alitangaza kuwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya chama hicho imeazimia kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano kote nchini kuanzia Septemba 1 ili kupinga udikteta unaoendelea hapa nchini.
Pia Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu amesisitiza jijini Dar es Salaam kuwa maazimio ya chama hicho yapo pale pale na kwamba maandalizi ya msingi ya utekelezaji wake yameanza.
“Hatutarudi nyuma, hatutatishika, wala hatutatetereka. Kwa siku chache UKUTA huu umekuwa imara hata kabla ya siku hiyo ya Septemba 1 na tumepokea salamu kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, taasisi na jumuiya mbalimbali wakitutia moyo juu ya jambo hili,” ameeleza.
Mwalimu amedai kuwa operesheni inayojulikana kama UKUTA ni mioyo ya watanzania wote na si chadema tu.
“Kufanya siasa ni wajibu wetu, siyo hisani ya mtu mmoja au kikundi cha watu. Ni wajibu wetu, ni haki yetu iliyo ndani ya sheria inayoongoza vyama vya siasa na kanuni zake,” aliongeza kwa kusema hayo Salumu Mwalimu.
Kwa upande wake Rais Dkt John Magufuli amesikika akiwa ziarani mkoani Singida akidai kuwa, “wanaotaka kuvuruga shughuli za maendeleo watakiona cha mtema kuni.”
Kauli hiyo inaonekana kuilenga Chadema pamoja na mpango wake wa kuendesha maandamano na mikutano hiyo nchi nzima.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.