EDWARD LOWASSA, FREEMAN MBOWE WATAKIWA KURUDI POLISI LEO



Viongozi wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana walikamatwa na Jeshi la Polisi wakati wakiwa katika kikao cha ndani katika Hoteli ya Giraffe mkoani Dar es Salam. 

Lowassa, ambaye alikaa kituoni hapo kwa takribani saa tatu anaweza kuwa kiongozi wa kwanza aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu kuhojiwa na polisi.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako baadhi ya wajumbe na wabunge waliwafuata na kuwasubiri nje ya kituo hicho kujua hatima yao. 

Viongozi hao walionekana wakiingia Polisi saa 10.30 jioni na kutoka saa 1.25 usiku, jambo ambalo liliwafanya wakae kituoni hapo kwa saa tatu. 

Lissu alisema polisi walivamia kikao hicho kilichokuwa na wajumbe 170, wakiwamo baadhi ya wabunge wa chama hicho na kuwakamata viongozi hao kwa maelezo kuwa wamekaidi amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na nje ya vyama vya siasa. 

Imeelezwa kuwa viongozi hao wa Chadema walikuwa na mkutano uliotanguliwa na kikao cha viongozi wakuu na kufuatiwa na cha viongozi hao kikijumuisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri. 

Wakiwa katika kikao hicho, ilielezwa kuwa watu wanne waliingia wakiwa wamevalia kiraia na kuwaeleza kuwa viongozi wao wanahitajika kituo kikuu cha polisi kutokana na kufanya mkutano kinyume cha sheria. 

Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza ambaye  alikuwa kwenye mkutano huo alisema pamoja na mambo mengine ya chama, walikuwa wakijadili suala la operesheni Ukuta la Septemba Mosi kama liendelee au lisiendelee kutokana na hali ilivyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwao, alisema viongozi hao walikamatwa kwa kukukaidi amri ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa na kuchochea wananchi kuandamana kinyume cha sheria Septemba Mosi. 

Alisema baada ya kuachiwa kwa dhamana, viongozi hao wametakiwa kuripoti kituoni hapo leo. 


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.