BAADA YA WAFANYAKAZI HEWA, SERIKALI YA JPM KUTENGENEZA AJIRA 71,496 HIVI KARIBUNI

Image result for job opportunities

Serikali ya JPM imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji wa wafanyakazi hewa. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki alisema,

“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.

Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa kwenye mfumo.


Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 16.

“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.

Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.

Alisema upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.

Pia alisema wameongeza kasi ili kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.

Alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.

“Baada ya kukamilisha mchakato huo, hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta ajira. 

"Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema. 






No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.