IMPORTANT!! TAARIFA KUTOKA HESLB: UFAFANUZI KUHUSU MADAI YA WASIOKOPA KUDAIWA MIKOPO ELIMU YA JUU
1.0 UTANGULIZI
Kumekuwepo na taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, hasa gazeti la Jamboleo toleo namba 2541 la 23 Agosti, 2016 kuhusu Bodi ya Mikopo kuwadai wasionufaika na mikopo. Taarifa hizi zinalenga kuleta hofu na mkanganyiko usiokuwa wa lazima kwa wadau. Kufuatia hatua hiyo Bodi ya Mikopo inapenda kutoa ufafanuzi wa suala hili kama ifuatavyo:-
2.0 MADAI KUHUSU KUDAIWA MIKOPO KWA WALE WASIONUFAIKA
Bodi ya Mikopo inapenda kuufahamisha Umma kuwa ‘database’ yake ya wanufaika wa mikopo ina taarifa zote muhimu zilizo sahihi. Hii inatokana na utunzaji mzuri wa kumbukumbu za ukopeshaji kuanzia hatua ya utoaji mikopo (loan allocation and disbursement) hadi urejeshaji wake (loan repayment). Kutokana hamasa na elimu inayotolewa, kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wanufaika wa mikopo na waajiri wao kujitokeza na kuanza kurejesha mikopo. Hivyo, katika utekelezaji wa jukumu hilo, tumebaini kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadaiwa kwamba ama hawakuwahi kukopa au hawajawahi kufikia kiwango cha elimu ya juu.
Hadi sasa, imebainika kuwepo kwa baadhi ya wanufaika ambao wanadai hawakujua iwapo fedha walizopatiwa na serikali wakati huo zilikuwa za mkopo. Pia kuna wachache ambao vyeti vyao vilitumiwa na ndugu zao kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu. Katika hali hii, mdaiwa atalazimika kumtaja mtu halisi anayepaswa kukatwa deni hilo ili Bodi iweze kusitisha makato hayo kwake.
Ili kupata ufumbuzi wa malalamiko hayo, Bodi inawataka walalamikaji kuzingatia yafuatayo:
2.1 Kwa mtu anayedai kwamba hajasoma elimu ya juu kwa ufadhili wa serikali au Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu; mtu huyu awasilishe vielelezo vinavyodhihirisha kuwa hakusomeshwa kwa ufadhili wa serikali.
2.2 Kwa mtu anayedai amekatwa mshahara ingawa hajawahi kufikia kiwango cha elimu ya juu; mtu huyo anapaswa kuwasilisha vielelezo vya kiwango cha elimu yake.
2.3 Iwapo kuna mnufaika wa mkopo anadai amekatwa zaidi ya kiwango cha mkopo anaodaiwa; mnufaika huyo anapaswa kuwasilisha vielelezo vinavyothibitisha kumaliza kurejesha deni lake. Itakapothibitika kuwa kuna makato zaidi yalifanyika, basi kiasi kilichozidi kitarejeshwa kwa mhusika.
3.0 HITIMISHO
Bodi inapenda kuwahakikishia wadau wake kuwa imetunza vizuri taarifa zote muhimu za wanufaika wa mikopo ambazo ndizo zinazotumika kwenye zoezi la urejeshaji wa mikopo. Kasoro ndogo ndogo zinazojitokeza zinatatuliwa kwa kufanya rejea kwenye kumbukumbu zilizopo.
Aidha, Bodi inaendelea kuwahimiza wanufaika wote wa mikopo ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao kuhakikisha wanawasilisha taaifa zao ofisi za Bodi au wanajaza taarifa zao kweye fomu ‘Loan Inquiry Form’ iliyopo kwenye tovuti ya Bodi na kuituma kwa anuani ya barua pepe info@heslb.go.tz ili kila mmoja ajulishwe deni lake na kuanza kurejesha.
Kwa mnufaika anayetaka kuanza kurejesha mkopo wake baada ya kuwa amepata taarifa ya deni lake; aweke fedha kwenye akaunti za Benki zifuatazo na kisha kuwasilisha hati ya malipo:
A/C No. 2011100205 – NMB
A/C No. 01J1028467503 – CRDB
A/C No. CCA0240000032 – TPB
Imetolewa na:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Agosti 24, 2016
No comments:
Post a Comment