MGOGORO WA CUF WACHUKUA SURA MPYA, LIPUMBA MATATANI KWA UPOTEVU WA MALI ZA CHAMA

Image result for LIPUMBA

Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, ili kumhoji mwenyekiti aliyerudishwa madarakani, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati wajumbe wa baraza hilo wakijiandaa kukutana kesho visiwani Zanzibar kutekeleza mpango huo, jana kutwa nzima, Profesa Lipumba alikuwa na kikao kizito na walinzi wa chama hicho (Blue Guard) makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ilisema baraza hilo, linamtaka Profesa Lipumba afike mbele ya kikao hicho ili  ajieleze na kujitetea kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia ofisi za makao makuu na kusababisha uharibifu wa mali.

“Kamati haijakubaliana na maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi juu ya Lipumba. Ilikutana jana (juzi)  kwa kikao cha dharura ofisi za Makao Makuu, Zanzibar na kujadili taarifa ya msajili,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo, ilisema  kamati pia ilijadili  kitendo cha uvamizi wa ofisi za Buguruni, kilichofanywa na Profesa Lipumba akiwa na kundi  la vijana ambao si wanachama wa CUF.

Alisema baada ya kikao kupitia maoni ya msajili, kamati iliamua kukataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni aliyoyapendekeza na badala yake inaendelea kusimamia maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalumu  Taifa uliofanyika Agosti 21, mwaka huu.

“Katika mkutano ule, wajumbe walikubali Lipumba kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama na katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa cha Agosti 28, mwaka huu, waliridhia kuwasimamisha uanachama Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye,” alisema.

Taarifa hiyo, ilisema Katiba ya CUF  haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusiana na uamuzi wa vikao vya chama na kubatilisha uamuzi wa vikao halali.

“Kutokana na kitendo cha kuvamia ofisi za Buguruni na kusababisha uharibifu wa mali za chama, kamati kwa mujibu wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka 2014 imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa Septemba 27, mwaka huu saa nne asubuhi ofisi za Zanzibar.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 , toleo la mwaka 2014, Kamati imeandaa ajenda ya kumfikisha Lipumba mbele ya Baraza Kuu na atatakiwa kujieleza na kujitetea kwa nini baraza lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake aliyoyafanya jana (juzi),” alisema.

Katika taarifa hiyo, Mazrui alisema ibara hizo zinaeleza juu ya kulinda heshima ya chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya Katiba, kutii kanuni za sheria na sheria ndogondogo za serikali iliyoundwa kihalali na.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba jana kutwa nzima alikuwa na kikao na walinzi wa chama hicho, (Blue Guard).

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilikuwa  na ajenda mbili ikiwamo ya kuimarisha ulinzi katika ofisi zote za chama na kujadili mali za chama ambazo ni pamoja na magari saba na kompyuta zilizoibwa wakati wa vurugu.


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.