RAIS MAGUFULI, AMPONDEA MAALIM SEIF KWA KUKATAA MKONO WA DK. SHEIN , ASEMA ANGEKUWA YEYE ASINGEWEZA KUVUMILIA HILO


Rais John Magufuli amemshangaa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuidhinisha fedha za matibabu ya mpinzani wake wa kisiasa, Maalim Seif Sharif Hamad wakati alikataa kumpa mkono wa salamu walipokutana kwenye mazishi wiki mbili zilizopita. 

“Mtu mmekutana kwenye msiba, mahali kwenye majonzi, mnamsindikiza marehemu. Kwa unyenyekevu wako Dk Dhein ukatoa mkono wako kumsalimia mtu fulani. Huyu mtu akakatalia mikono yake na bado asubuhi yake ukasaini fomu zake za kwenda kutibiwa nje ya nchi?” alisema Magufuli. 

“Haya ni mapenzi makubwa sana. Amekataa mkono wako. Huyohuyo akiugua unampeleka hospitali. Akitaka kusafiri nje, unasaini na unampa na fedha na posho za kwenda nje. Mimi nisingeweza.” 

Rais ametoa kauli hiyo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kisiwani Unguja ambako amekwenda kushukuru wananchi kwa kumchagua kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita. 

Uhasama ulifikia kiwango cha juu wakati Maalim Seif alipokataa kumpa mkono Dk Shein walipokutana kwenye mazishi ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi kitendo kilichomfanya Rais Magufuli aeleze yake ya moyoni jana. 

Akishangiliwa na wananchi, ambao wengi walivalia fulana za rangi za njano na kijani ambazo hutumiwa na CCM, Rais Magufuli alisema Dk Shein ni mpole na kama angekuwa na moyo kama wake, hali ingekuwa tofauti baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha Maalim Seif. 

“Niutoe mkono wangu, uukatae halafu kesho niende ofisini kukusainia wewe (akaongea kilugha). Ndiyo maana nasema wewe ni special. Nafikiri wanapotoka malaika wewe ndiyo unafuata. Kama mtu anaukataa mkono wako, na wewe kataa kufanya mambo yake, ajifunze kwamba na wewe mkono wako una thamani.” 

Alisema anaomba Mungu amsaidie kumpa angalau nusu ya moyo wa Dk Shein na kuomba Mungu ampe Dk Shein nusu ya roho na mawazo yake ili Zanzibar iende bila kelele za aina yoyote. 

“Jana nilikwambia angalau uongeze kaukali kidogo. Umefanya mambo makubwa sana katika nchi hii. Tulishazungumza na wewe umezungumza kwamba kwa mujibu wa Katiba, uchaguzi umekwisha, ukisharudiwa umekwisha. Utarudiwa tena mwaka 2020, wazunguke waimbe lakini wewe ndiye rais,” alisema. 

Magufuli alisema upendo na unyenyekevu alionao Dk Shein ni wa hali ya juu kwani licha ya mikikimikiki aliyoipata kutoka kwa wapinzani, ameendelea kuwaingiza katika Serikali yake, jambo ambalo yeye hawezi kulifanya. 

“Mimi nilipata ushindi kwa asilimia 58, lakini hakuna mtu kutoka chama kingine atakayekanyaga mguu kwenye Serikali yangu. 

"Mzee huyu ana moyo wa tofauti, namuomba Mungu apate hata robo ya moyo wangu maana amekuwa mpole mno,” alisema Dk Magufuli. 
 

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.