RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE ATUNUKIWA TUZO YA UONGOZI WA KISIASA NA UTETEZI
Shirika lisilo la Kiserikali la Speak Up for Afrika limemtunukia tuzo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
Utoaji wa Tuzo hiyo ya uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Speak up Afrika. Hafla hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York ilikuwa pia ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji wa shughuli za Taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa na Speak Up Afrika, taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa Karibu na Rais Mstaafu Kikwete, ni katika maeneo ya upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto, udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia kampeni ya malaria haikubaliki ,usambazaji wa vyandarua vyenye viatilifu, kampeni ya lishe bora, na kampeni ya chanjo kwa watoto.
Pamoja na kutambua juhudi za Rais Mstaafu Kikwete katika kuyasemea maeneo hayo, Taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kulisema Bara la Afrika kila mara alipopata fursa ya kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Rais kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwaajili ya watu wenye mahitajio ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
Akipokea Tuzo hiyo, Rais Mstaafu Kikwete , amesema Tuzo hiyo ni ya watoto wote waafrika ambao ndio waliomfanya asimame mbele ya wageni waalikwa.
“ Ni kwa sababu yenu ndio sababu nimetenga muda wangu baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya kuboresha maisha yenu. Ninafanya hivyo kwasababu makuzi yangu yalikuwa kama ya mtoto yeyote yule wa kiafrika, nimeyaishi maisha wanayo ishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika hamu na kiu yao ya kuwa na maisha bora na afya njema”. Akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.
No comments:
Post a Comment