ACHANA NA TUKIO LA ROMA... LINGINE LIMETOKEA
DAR ES SALAAM: Huku tukio la msanii wa Hip Hop, Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ na wasanii wenzake watatu kutekwa studio likiwa bado halijapoa, mwinjilisti aliyefahamika kwa jina la Onoratus Mwinuka (51), mkazi wa Mabwepande jijini Dar, amedaiwa kutekwa na kuuawa kisha mwili wake kufukiwa ardhini huko Mabwepande, Risasi Jumamosi linakudadavulia.
HABARI KAMILI Kwa mujibu wa dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Veronica Mwinuka, taarifa za kupotea kwa kaka yeka alizipata Machi 14, mwaka huu kutoka kwa watoto wa marehemu ambapo walisema tangu baba yao alipoondoka alfajiri ya Machi 13, mwaka huu hakuwa amerejea tena nyumbani.
Veronica aliendelea kusema watoto hao walimwambia pia katika alfajiri hiyo ya saa kumi, marehemu aliondoka na mfanyakazi wake wa kiume aitwaye Ayubu aliyekuwa na kawaida ya kumsindikiza kila mara kutafuta usafi ri ili apeleke maziwa ya ng’ombe mjini kisha akishapata usafi ri yeye hurudi nyumbani.
Inadaiwa kuwa, siku hiyo, walipofi ka kituoni, lilitokea gari aina ya Toyota Noah, wakamuuliza marehemu kama anakwenda, akakubali na kupanda, gari likaondoka.
“Baada ya hao watoto kunipa taarifa hizo sikuweza kushituka mara moja maana nilifahamu pengine kaka alikuwa amepitia kwenye shughuli zake nyingine za kiuinjilisti maana alikuwa ni muinjilisti lakini baada ya kupita siku hiyo aliyopotea, siku iliyofuata kuna wizi ulitokea nyumbani kwake ndipo nikashituka,” alisimulia Veronica.
WIZI WATOKEA NYUMBANI KWA MAREHEMU
Veronica aliendelea kusema kuwa, wizi huo uliofanyika ulifanywa na mmoja wa wafanyakazi wa marehemu ambaye aliiba fedha zinazokadiriwa kufi ka shilingi milioni 30 ambazo marehemu alikuwa amezitoa benki siku moja kabla ya kupotea kwake kwa ajili ya kununua gari ndogo (pick up) ya mizigo na kuwalipia wanaye ada ya shule.
“Kiukweli niliona si hali ya kawaida hasa nilipounganisha matukio ya kuibiwa nyumbani na kupotea kwake.
“Lakini mbaya zaidi kaka nyumbani alikuwa amebaki mwenyewe. Mkewe alikuwa nyumbani kwao kwa ajili ya kumuuguza mdogo wake, kwa hiyo niliamua kuwataarifu ndugu zangu wengine, akiwemo shangazi yetu ambapo akatutaka tutoe taarifa kwenye vyombo vya usalama.”
ATAFUTWA MPAKA MOCHWARI
“Mkewe pia alirudi, tukaenda kwenye ofisi za serikali ya mtaa kisha kwenye Kituo cha Polisi Mabwepande ambako tulitoa taarifa na kupewa RB ili kumtafuta yeye pamoja na mfanyakazi yule aliyeiba.
Kazi ya kumtafuta sehemu mbalimbali ikaanza ikiwemo mahospitalini, mochwari na sehemu nyingine mbalimbali lakini hatukuweza kumpata kaka kwa zaidi ya siku ishirini baadaye,” alisema Veronica.
AZIDI KUSIMIULIA
Dada huyo wa marehemu aliendelea kusema kuwa, ilifi ka hatua ndugu wakakata tamaa kwamba hawezi kupatikana tena, lakini hivi karibuni mdogo wao mwingine wa mwisho aitwaye Alphonsia Mwinuka alifi ka kutoka Mbozi, Mbeya kwa ajili ya kazi hiyo ya kumtafuta kaka yao.
Baada ya kufi ka akishirikiana na kijana wa kazi (Ayubu) aliyekuwa na marehemu siku ya mwisho kuonekana pamoja na watoto wa marehemu, walianza msako upya katika misitu inayozunguka nyumba ya marehemu.
SIKU YA MWILI KUONEKANA
“Kiukweli siku hiyo tulimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. Giza lilipoanza kuingia mimi nilikuwa tayari nimechoka, nikamwambia Ayubu pamoja na mtoto wa marehemu aitwaye Daniel mwenye miaka kama saba kwamba, waende upande mwingine kumtafuta mimi nikarudi nyumbani.”
DALILI ZA KUONEKANA MWILI WA MAREHEMU
“Baada ya muda walirudi na kuniambia kuna sehemu porini ilichimbwa, pia ilikuwa na ufa jambo lililoashiria kwamba kuna kitu kilizikwa.
Ayubu alisema alipatilia shaka hivyo kupapiga picha kwa kutumia simu yake ya kisasa (smart phone). “Baada ya kunionesha na mimi zile picha niliitilia shaka ile sehemu.
Lakini sikuongea jambo lolote mpaka siku iliyofuata, tulitoa taarifa kwenye vyombo vya usalama na kwenda kwenye eneo lile tukiambatana na wananchi wa mtaa ule, lengo ni kuangalia pale mahali palizikwa nini,” alisema Alphonsia.
ENEO LA TUKIO
Alphonsia alisema, walipofi ka jirani na eneo hilo aliloliona kwenye picha mnato za simu, cha kushangaza, yule kijana akaanza kuwazungusha, lakini baada ya kumbana aliweza kuwaonesha na baada ya kuchimba waliukuta mwili wa marehemu ukiwa umeharibika sana.
“Kiukweli ilitusikitisha mnomno, hatukuweza kuamini kuwa mwili tuliokuwa tunauona ulikuwa ni wa ndugu yetu, hasa baada ya mkewe kuyatambua mavazi. Kutokana na tukio lenyewe ilionesha ndugu yetu alitekwa na watu waliomuua kisha wakamzika pale.
“Ni vigumu kufahamu sababu hasa ilikuwa nini lakini ni jambo lililoibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu. “Baadaye polisi walipokuja, walimchukua Ayubu kwa ajili ya kwenda kusaidia upelelezi na mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya taratibu zingine za kipolisi,” alisema Alphonsia.
TAMKO LA SERIKALI YA MTAA
Naye mwenyekiti wa mtaa huo, Abdallah Omar alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alilaani vikali matukio ya utekaji nyara yanayoendelea nchini na kusema ni kinyume na haki za binadamu. Mwili wa marehemu ulizikwa juzi Alhamisi kwenye Makaburi ya Mabwepande. Ameacha mke na watoto wanne.
KUMBUKUMBU MUHIMU
Matukio ya utekaji yanazidi kushamiri nchini, hadi sasa rekodi inaonesha, waliowahi kutekwa ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane (hajapatikana), aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, Absolom Kibanda (alijeruhiwa), Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka (alijeruhiwa) na Roma Mkatoliki (alijeruhiwa) na wenzake watatu.
Hata hivyo, baadhi ya matukio hayo yamekuwa yakihusishwa kufanywa na wabaya wa waathirika hao ambapo baadhi ya wabunge, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, hivi karibuni alitoa hoja ya kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguzaa matukio hayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kwa upande wake alisema serikali inachunguza matukio hayo ili kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment