MAHAKAMA YAKUBALI OMBI LA KUWASAFIRISHA WATANZANIA WATATU WANAOTUHUMIWA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA KWENDA NCHINI MAREKANI KUSIKILIZA TUHUMA ZINAZOWAKABILI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali maombi ya Waziri wa Katiba na Sheria ya kuwasafirisha watanzania watatu  wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwenda nchini Marekani kusikiliza tuhuma zinazowakabili.

Hakimu Mkazi mfawishi Cyprian Mkeha ametoa uamuzi huo leo. Wajibu maombi hao ni Ally Hatibu Hassan maarufu kama Shkuba, Iddi Salehe Mafuru, na Lwitiko Emmanuel Adam.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkeha amesema, wajibu maombi hao watakaa rumande hadi kibali kutoka kwa Waziri wa Katiba na Sheria kitakapotolewa. Aidha mahakama imesema kuwa wajibu maombi wanahaki ya kukata rufaa ndani ya siku 15 kabla ya Waziri wa katiba na Sheria hajatoa Kibali cha  kuwasafirisha.

Mapema wiki hii Waziri wa Katiba na Sheria  kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Edwin Kakolaki aliwasilisha maombi ya kuwasafirisha wajibu maombi hao kwenda nchini humo kujibu tuhuma za kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya.

Katika maombi hayo, wajibu maombi wanadaiwa kuhusika kwenye njama za kusafirisha na kusambaza zaidi ya kilo moja ya Heroine nchini humo.

No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.