UTOFAUTI UNAOLETA UTOFAUTI, TABIA KUU 5 ZA WATU WALIOFANIKIWA ZAIDI..
HIZI HAPA TABIA KUU TANO ZA WATU WALIOFANIKIWA ZAIDI, UTOFAUTI UNAOLETA UTOFAUTI, ( THE DIFFERENCE THAT MAKES THE DIFFERENCE)
Kwanza, kabla sijaendelea embu tuwekane sawa kuhus hii falsafa ya “kufanikiwa kimaisha”, ina maana gani haswa? Ukweli ni kwamba watu wengi wakisikia fulani amefanikiwa kimaisha, basi moja kwa moja wanafikiri au wanaamini mtu huyo atakuwa na pesa nyingiiii au kwa maneno mengine, mtu huyo ni tajiri fulani hivi. Pamoja na kwamba pesa ndio mtatuzi wa mahitaji mengi hapa duniani, lazima tukumbuke kwamba pesa ina uwezo wa kununulia kitanda cha gharama kubwa sana, lakini ukashindwa kulala katika kitanda hicho kwa msongo wa mawazo. Pia pesa inaweza ikakufanya uopoe mwenza mzuri kuliko wote duniani, lakini mwenza huyo asiwe na mapenzi ya dhati kwako.
Hapa tunajifunza kwamba ingawa pesa ni muhimu sana maishani, kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mtu kimaisha hakuwezi kupimwa kwa kiasi tu cha pesa alichonacho. Mtu anaweza akawa na pesa, lakini akakosa raha kutokana na ukosefu wa amani ya ndani na nje ya mwili. Hivyo basi, Kufanikiwa au kutofanikiwa maishani kwa mtu, ni lazima pia kupimwe kwa mambo mengine muhimu kama uchamungu, ukarimu, maadili, busara, uvumilivu, na ujasiri (wa kufanya na kuishi na maamuzi magumu). Hivi “viambatanisho” 6 vya pesa ndio vinarutubisha na kudumisha pesa, na zaidi humfanya mtu afurahie (enjoy) pesa hizo. Kwa uzoefu wangu, mchanganyiko wa mambo haya yote muhimu, ndio humfanya mtu “afanikiwe kimaisha” kwa maana pana ya falsafa hiyo. Baada ya muhtahsari huu, tuendelee sasa na mada yetu, ambayo leo inagusia mambo makuu matano ya watu waliofanikiwa kama ifutavyo:
#1: Huishi Kwa Siku Za Baadae (Future), Na Sio Siku Zilizopita (Past). Bila shaka umeshasikia ule usemi wa siku nyingi kwamba “yaliyopita si ndwele, tugange yajayo”. Watu waliofanikiwa kimaisha huwa na tabia ya kutokatishwa tamaa na mambo ambayo yameshapita, na hayakwenda kama walivyotarajia, kwani siku zote huwa wanakubali matokeo ya kutofanikiwa kwao katika suala fulani na kujipanga upya kulikabili suala hilo. Siku zote hujizuia kuruhusu matukio ya kushindwa kwao kufanikiwa katika masuala fulani maishani, kushusha imani yao yakufanikiwa katika masuala ya baadae (future).
#2: Hawalii Shida Na Wala Hawana Kinyongo. Hisia zako za siku kwa kiasi kikubwa zinategemea na wapi ulipoelekeza mawazo yako. Kwa mujibu wa mtaalam wa Saikolojia, Travis Bradberry, anaweka wazi kwamba “kama umeelekeza mawazo yako kwenye shida ambazo zinakukabili, basi unajijengea hisia hasi mwilini na kujiongezea mastresi kibao, ambayo yana athiri na kuzuia uwezo wako wa kufanya mambo ya kimaendeleo”. Hivyo basi, watu waliofanikiwa maishani huwa wanaelekeza mawazo yao kwenye masuala chanya, ili kupiga vita mastresi na kujiongezea uwezo wa kukomaa na mambo ya maendeleo. Pia, watu waliofanikiwa maishani huwa hawaendekezi kinyongo, kwani wanaelewa kuwa kuweka kinyongo katika masuala yaliyopita ni hatari sana kwa maendeleo. Vinyongo kama ilivyo kubebea shida mbeleko, ni vitu ambavyo huzalisha hisia hasi mwilini na kumfanya mtu kuwa na mastresi (au msongo wa mawazo), ambayo yana mzuia kufanya mambo ya maendeleo.
#3: Hawatoi Kipaumbele Katika Ukamilifu. Hapa ina maanisha kwamba, watu waliofanikiwa maishani huwa hawapotezi muda katika kutafuta ukamilifu (perfection) katika mambo yao. Ni watu, ambao wanafaham kwamba binaadam ni viumbe dhaifu na ukamilifu ni wa Mungu peke yake. Hivyo basi, hii sifa inawasaidia sana linapokuja suala la kuridhika na kile walichoweza kufanya baada ya kujitahidi kwa uwezo wao. Hii inawafanya waendelee kujiamini, badala ya kujilaumu na kujihisi wamefeli kama wale watu wanaolenga ukamilifu katika ufanyaji wa mambo yao.
#4: Hawapotezi Muda Wao Na Watu Wenye Mawazo Hasi. Hii sifa ni muhimu sana na kwa ufupi ni muendelezo wa sifa #2, kwani ili mtu aendelee kubaki na mawazo chanya kwa mustakbali mzima wa maendeleo yake, ni lazima apinge kukaa na watu wenye mawazo hasi au walalamikaji. Kwa ung’eng’e wanasema “ don’t hangout with negative people!” Hapa wanazungumziwa marafiki, ndugu, na jamaa, yaani kuwa makini sana kuhusu watu unaokaa na kuzungumza nao kwa siku. Kama watu hawa wamejaa malalamiko tu kuhusu maisha yao siku nzima, basi jua wanagonjwa hatari sana na ni watu wa kukaa nao mbali, ili wasikuambukize gonjwa hilo hatari kwa maendeleo yako. Siku zote watu waliofanikiwa maishani (au wale walio mbioni kufanikiwa) huwa wanajihusisha na watu wenye mawazo chanya na matumaini tele kuhusu mustakbali wa maisha yao.
#5: Hawaoni Hatari Kusema “Hapana!” Hii pia ni sifa muhimu sana, kwani watu wengi wanaostrago maishani, ni watu ambao wanataka kumridhisha kila mtu, kitu ambacho ni kigumu sana. Mbali na kwamba sifa moja wapo ya mtu aliyefanikiwa maishani ni ukarimu, watu hawa pia wana ujasiri wa kusema hapana katika mambo ambayo hawataki au hawana muda wa kufanya. Ni watu ambao hawazunguki mbuyu linapokuja suala la kumwambia mtu kwamba ombi lao kwao limekataliwa. Hapa sio tu kwa wale watu wanaopenda kupiga mizinga ya pesa (ambayo mengine haina msingi wowote), bali pia kusema hapana linapokuja suala la kuombwa msaada wa kikazi na washirika wa biashara au ajira. Watu waliofanikiwa maishani hawaoni hatari kukataa kutoa msaada wa kikazi kwa watu wengine, ili kujipa muda zaidi na uwezo wa kufanya kazi zao.
Anza kufanya uchunguzi wako leo kwa watu unaowafaham, ambao “wamefanikiwa maishani” na utaona mifano hai ya sifa hizi au kama tayari unawafaham watu hao, basi tupe maoni yako kwa faida ya wasomaji wote!
Rungwe Jr.
No comments:
Post a Comment