MAKONDA, SIRRO WAITWA MAHAKANI LEO ,, NI KESI ALIYOFUNGUA MBOWE DHIDI YAO


Image result for makonda na sirro

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, wamepelekewa barua za mwito za kuwataka wafike Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo.

Viongozi hao wamepelekewa mwito huo kutokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe dhidi yao.

Mbowe amefungua kesi hiyo kupinga Makonda kumtaja katika orodha yake ya watuhumiwa 65 wanaojihusisha na dawa za kulevya katika awamu ya pili na kumtaka afike katika Kituo Kikuu cha Polisi, Februari 10 mwaka huu, kwa ajili ya mahojiano.

Katika kesi hiyo Namba Moja ya Mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo mengine, anapinga mamlaka ya RC kumkamata kwa kile anachokiita kudhalilisha watu.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa leo na itasikilizwa na jopo la majaji watatu, Sekieti Kihiyo ambaye ni kiongozi wa jopo hilo, akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday.

Mbowe anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa vifungu vya Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa vinavyowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume cha Katiba.


No comments:

This Website Is Developed & Maintained By Jesse. Powered by Blogger.